
Wasanii vinara wa muziki wa Kizazi kipya nchini, Rashid Abdallah ’Chid Benz’ na Khaleed Mohamed ‘Tid’, hivi karibuni wamechapana makonde laivu...

Ilidaiwa kuwa, awali Chid akiwa na rafiki zake wawili alitinga ukumbini hapo na kwenda kupozi karibu na DJ aliyekuwa akisababisha vilivyo huku wakiwa na ‘monde’ (kinywaji) mkononi.
Chanzo kilisema kuwa, haukupita muda mrefu ‘Top In Dar’ naye alitinga ukumbini humo akiwa na kundi lake wakiwa ‘fulu kinywaji’, ambapo moja kwa moja walikwenda kunakouzwa ‘moja baridi, moja moto’ (kaunta) na kuketi.
Huku akizungukwa na warembo waliokuwa wakimtaka akacheze nao muziki, TID alishutushwa na kundi lililoongozwa na Chid, lililovamia warembo wale, kisha kumtishia kumshushia kichapo mkali huyo maarufu kama sauti ya gerezani.
Chanzo kiliendelea kusema kuwa, TID hakuwa tayari kukutwa na fedheha hiyo mbele ya ‘totozi’ hivyo alilazika kuonesha maujuzi ya kurusha ngumu aliyolambishwa toka gerezani.
Ilisemekana kwamba, Chid kama kiongozi wa kundi lake, naye alijikuta akionesha ubabe wa ‘kitaa’ pale alipomrukia TID na kujikuta wakizichapa kavukavu.
Baada ya vurugu hilo ambalo lilikuwa ni soo tupu, mabaunsa wa ndani ya kiwanja hicho walilazimika kuingilia kati kuamulia ngumi hizo zilizokuwa zikirushwa na mastaa hao kama mvua ya mawe.
Katika timbwili hilo, TID alisikika akidai kuwa, haogopi jela, hivyo alitaka kumuonesha Chid ‘mbivu na mbichi’ siku hiyo hadi aite maji ‘mma’.
Hata hivyo, kiongozi wa mabaunsa hao (jina tunalo) aliamuru TID na Chid watolewe nje ya ukumbi huo, kisha kufungiwa kabisa kutinga katika kiwanja hicho cha maraha.
Mwandishi wetu alifanya juhudi za kutaka kujua kama kweli wanamuziki hao wamefungiwa kutinga Club Billicanas, kiongozi mmoja wa mabaunsa ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alithibitisha kutokea kwa ugomvi huo na kufungiwa kwa wasanii hao kutinga ukumbini hapo.
Alipotafutwa TID katika simu yake ya mkononi ili kuzungumzia ‘ishu’ hiyo, alikubali kutokea kwa tukio hilo siku hiyo lakini aliomba isiwe ‘stori’.
“Dah ile ishu ilikuwa ni noma lakini wana isiwe stori ikaushieni siyo kivile,” alisema TID.
Juhudi za kuongea na Chid ziligonga mwamba kufuatia simu yake ya kiganjani kutopokelewa kila ilipopigwa.
Chid ambaye mwaka huu ametwaa tuzo ya mwanahiphop bora kupitia wimbo wake wa ‘Ngoma itambae’, aliwahi kuripotiwa tena kutwangana na mkali mwenzake, Joseph Haule ‘Profesa Jay’.
Naye TID, hivi karibuni ametoka jela alipokuwa akitumikia kifungo cha mwaka mmoja baada ya kukutwa na kosa la kumpiga dogo mmoja wa kitaa na kumsababishia maumivu makali.
No comments:
Post a Comment