KARIBU SANA

Thursday, January 8, 2009

Kill Stars inatisha

Mshambuliaji wa Kilimanjaro Stars, Danny Mrwanda akichuana vikali na nahodha wa Rwanda,Nsutuyamagara Ismael katika moja ya heka heka za Kombe la Chalenji. Stars ilishinda 2-0.

IKICHEZA soka safi na la kujiamini lililowalazimisha Waganda kuishangilia, Kilimanjaro Stars ilitandika bila huruma Rwanda kwa mabao 2-0 na kujisafishia njia, wakati wapinzani wa Uganda wakisambaratisha Somalia 4-0.

Ushindi huo umeifanya Stars kufikisha pointi sita na kuongoza kundi kwa muda, huku kiungo wake, Athuman Idd akinyemelea ufungaji bora kwa mabao mawili aliyonayo.

Stars ambayo ilianza mchezo huo kwa kushambulia kwa nguvu, iliandika bao la kwanza dakika ya nane kupitia kwa winga wake Mrisho Ngassa ambaye alipiga 'tiktak' iliyogonga besela na kutinga wavuni.

Rwanda ambayo ilicheza soka la pasi nyingi fupi fupi na kushambulia kwa kushtukiza, ilijipanga na kupandisha shambulizi kali dakika ya 10 na kupangua ukuta wa Stars, lakini Lomani Jean akachachawa na kupaisha.

Washambuliaji wa Stars walizidi kuishambulia Rwanda, ambapo dakika 23 Henry Joseph alipiga shuti kipa akatema, lakini Mrisho Ngassa akaichelewa kumalizia.

Stars ambayo wachezaji wake walikuwa wakikaba kwa nguvu, kwa kujiamini na kutowapa nafasi Rwanda

kukaa na mpira, ilizidi kushambulia huku wachezaji wake wakionana vizuri na kuandika bao la pili dakika ya 37 kupitia kwa Athuman Iddi 'chuji'.

Iddi ambae katika siku za hivi karibuni amekuwa akianza benchi, alishangiliwa na Waganda baada ya kufunga goli hilo safi kwa kupangua ukuta wa Rwanda na kupiga shuti kali lililomshinda kipa huyo namba mbili, Rutayisire Patrick.

Stars ambayo wachezaji wake Haruna Moshi, Godfrey Bonny na Shadrack Nsajigwa walionyeshwa kadi, ilicheza soka la kuvutia ambalo liliwazimu washabiki wa Uganda kuishangilia muda wote wa mchezo.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ile ile, huku Danny Mrwanda na Mrisho Ngassa wakiwa kivutio kikubwa kutokana na kushambulia kwa kasi na kuwatoa jasho mabeki wa Rwanda ambao walilazimika kutumia nguvu nyingi na ubabe.

Watanzania walizidi kukaba kiumakini huku uzio wa mabeki Shadrack Nsajigwa, Salum Sued na Kelvin Yondani ukionekana imara zaidi kutokana na kuokoa hatari nyingi za mshambuliaji Kamana Bokota.

Washambuliaji wa Rwanda, Gasana Eric, Bokota na Lomani Jean walikuwa wakitengeneza pasi nzuri, lakini wakashindwa kupenya ukuta wa Stars na pale walipofanikiwa kupenya wakajikuta wakipaisha au mashuti yao kupanguliwa na kipa Deo Boniventure

'Dida' ambaye alionyesha ustadi. Stars imesaliwa na mchezo mmoja dhidi ya Uganda hapo kesho Ijumaa kwenye uwanja wa Nakivubo, huku Rwanda ikikwaana na Zanzibar yenye pointi nne.

Kocha Marcio Maximo alimtoa Athuman Idd, Mrisho Ngassa na Haruna Moshi kipindi cha pili na kuwaingiza Nizar Khalfan, Mussa Mgosi na Nurdin Bakar ambao nao waliendeleza mashambulizi kama ilivyokuwa awali.

Baada ya mchezo huo kocha wa Stars, Marcio Maximo alisema kwamba alijua Rwanda ni wagumu ndio maana akawaelekeza wachezaji wake kukaba kwa nguvu mwanzo mwisho.

"Nilijua itakuwa ngumu ndio maana nikawaambia wasimuachie mtu acheze mpira, wao wanauzoefu wa kumiliki zaidi kuliko sisi na nashukuru wachezaji wangu wamenielewa ndio maana tumeshinda,"alisema Mbrazil huyo.

"Ninachoangalia sasa ni kupanga kwa mashambulizi kwa mchezo ujao najua utakuwa mgumu sana kwa vile Uganda wako imara na wako nyumbani."

Kocha wa Rwanda ambayo ina pointi tatu, Branco Tucak alisema kwamba anajipanga kwa mchezo ujao dhidi ya Zanzibar, lakini akasifu jinsi Stars ilivyokuwa ikikaba vizuri.

Katika mchezo wa pili Uganda iligeuza hasusa Somali kwa kuitandika mabao 4-0 huku mshambuliaji Tony Maweje akipachika mabao mawili pekee yake.

Mabao mengine ya wenyeji hao yalifungwa na Owen Kasule dakika ya 31 na Masa Godfrey katika dakika ya 74 kwenye mchezo huo uliokuwa wa upande moja tu.

Kikosi cha Stars; Deo Boniventure, Shadrack Nsajigwa, Juma Jabu, Salum Sued, Kelvin Yondani, Godfrey Bonny, Mrisho Ngassa/Mussa Mgosi, Henry Joseph,Danny Mrwanda, Haruna Moshi/Nizar Khalfan na Athuman Idd/Nurdin Bakar.

No comments:

Post a Comment