KARIBU SANA

Saturday, December 6, 2008

Zitto amshutumu Waziri Malima kwa kumpinga Spika


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, amesema kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adamu Malima, hakupaswa kutoa kauli ya kumpinga Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samwel Sitta, kuhusu uwazi kwenye mikataba ya madini.

Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alitoa kauli hiyo jana kwenye Viwanja vya Sahara, wakati akihutubia wananchi wa Jiji la Mwanza kwenye Operation Sangara.

Alisema Malima hakupaswa kumjibu wala kumpiga Spika Sitta kuhusu mikataba ya madini kuwekwa wazi na kupelekwa bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na wabunge, kwa sababu inahusu rasimali ya taifa.

Alisema kauli ya Malima juu ya mikataba hiyo kuhusiana na mambo ya biashara haina mantiki yoyote, kwa sababu wawekezaji wanaokuja kuwekeza wanawekeza kwenye ardhi ya Watanzania na wanachochuma ni rasilimali ya yao, hivyo wanapaswa kuijua mikataba inayotiwa saini na Serikali.

Zitto alisema Malima hakupaswa kumjibu Spika kutokana na umri wake na nafasi ya uspika aliyonayo katika nchi hii na kusisitiza kwamba, kwa kauli yake ameonyesha kushindwa kumheshimu spika na muhimili muhimu nchini.

“Spika anaongoza wabunge zaidi ya 360 na bunge ndicho chombo cha kutunga sheria na kuisimamia serikali, hivyo kauli ya Wziri Malima inaonyesha jinsi asivyoli liheshimu bunge ambalo ni muhimili muhimu katika nchi hii,’ alisema na kuongeza:

“Hivi Malima ni nani katika nchi hii ambaye anaweza kupingana na kauli ya Spika ya kutaka mikataba ya madini inayotiwa saini na serikali kufanywa kwa uwazi na kupelekwa bungeni. Hivi jeuri hiyo ya kumjibu Spika ameitoa wapi?”

Alisema kuwa yeye binafsi anakubaliana na kazi kubwa inayofanywa na spika na anaiunga mkono, kwa sababu ameleta mabadiliko makubwa katika bunge hadi kufikia hatua ya Waziri Mkuu wa nchi kujiuzulu kutokana na kutowajibika.

Alisema kutokana na hali hiyo ni lazima suala la mikataba ya madini lifanyike kwa uwazi kwa sababu ni mali ya Watanzania, hivyo hakuna sababu ya kufanywa kwa siri.

Aidha, Zitto alisema kuwa inasikitisha kuona walimu wanalalamikia serikali kwa kushindwa kuwalipa madai mbalimbali yakiwemo malimbikizo ya mishahara, huku serikali ikisamahe mabilioni ya fedha kwa wawekezaji wanaomiliki kampuni mbalimbali za madini hapa nchini.

Alisema kutokana na hali hiyo, ni wazi kuwa serikali imeshindwa kusimamia ipasavyo rasilimali za nchi na kuwafanya watu kutoka nje kunufaika na utajiri wa nchi wakati Watanzania wakiendelea kuwa masikini.

“Ndugu zangu hakuna mtu anayekataa wawekezaji hata mimi nawakubali, lakini ambao hawalipi kodi na ambao wanaochukua rasilimali zetu bila ya taifa kupata chochote hawanafaida kwetu na hakuna sababu ya nchi kuwa na wawekezaji wa aina hii,” alisema Zitto.

No comments:

Post a Comment