KARIBU SANA

Saturday, December 6, 2008

Malinzi sasa kupambana na Tenga TFF


KAMATI ya Rufaa ya Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji John Mkwawa imepitisha jina la Jamal Malinzi kuwania nafasi ya urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa TFF, utakaofanyika Desemba 14 katika Ukumbi wa NSSF WaterFront jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Kamati hiyo ya Rufaa, Mtemi Ramadhan alisema jana kuwa wamempitisha Malinzi kuwania nafasi hiyo baada ya kamati kuridhishwa na vielelezo vya ziada ambavyo Malinzi hakuviwasilisha mwanzoni katika Kamati ya Uchaguzi ya TFF.

Kutokana na uamuzi huo, Malinzi sasa atapambana na mgombea pekee anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga ambaye tayari amejinasibu kuwa anastahiki kuendelea kwa kuwa wamekwishajenga msingi.

“Siyo kwamba kamati iliwaonea hapana ni kweli Malinzi alikuwa hajakidhi vigezo katika Kamati Kuu ya Uchaguzi wakati wanamfanyia usaili,’’ alisema Mtemi.

Alisema kuwa Malinzi katika vigezo vyake vya awali vilikuwa vinaonyesha ametumikia soka kwa miaka minne tu kitu ambacho katika kipengele cha kuwania uongozi huo, lazima awe ametumikia soka katika miaka mitano, lakini katika Kamati ya Rufaa alileta vielelezo vyote na kuthibitisha kuwa alikuwa mjumbe wa bodi ya ushauri ya Yanga kwa kipindi cha mwaka mmoja na kufikisha miaka mitano.

Alisema kwa upande wa Michael Wambura mgombea wa nafasi ya Makamu wa kwanza wa Rais, kamati imeamua uamuzi wa rufaa yake utatolewa kwenye kikao kijacho kitakachofanyika Desemba 10 baada ya kamati kujiridhisha na vielelezo atakavyovitoa kama alivyoagizwa na kamati.

Mtemi, mchezaji wa zamani wa Simba, alisema kuwa kamati hiyo imemtaka Wambura awasilishe nyaraka za fedha wakati alipokuwa kiongozi katika shirikisho hilo, pia, kamati inachunguza uhalali wa nyaraka alizoziwasilisha kwa kamati.

Hata hiyo, kamati hiyo ilikubali rufaa zilizotolewa na wagombea wanne waliokuwa wanawania ujumbe katika kamati hiyo ambao ni Israel Mwansasu ambaye amejitoa.

Alisema kwa upande wa Khalid Abdallah anayewania Ujumbe wa kamati ya utendaji, kamati imeamua kumrejesha baada ya kuridhika na vielelezo vya ziada kama ilivyo kwa Murtaza Mangungu.

Wengine waliopita ni Lameck Nyambaya ambaye naye amerejeshwa baada ya kamati kuridhika na Mulamu Nghambi ambaye anatakiwa kufanyiwa usaili na kamati ya uchaguzi Desemba 10 kwa kuwa hakuwepo Novemba 26 wakati wagombea wakifanyiwa usaili.

Katika hatua nyingine, mgombea aliyekatwa katika usaili Michael Wambura amesema kuwa hana imani na kamati ya rufaa na anahisi hujuma ili asiingie katika uchaguzi huo mkuu wa TFF.

Wambura alisema: “Sijui mpaka sasa ni kitu gani kinaendelea katika kamati hiyo kwani hoja yao ya kwanza ilikuwa sijakabidhi ofisi na baada ya kujulikana nimekabidhi wanaleta hoja nyingine ya kukabidhi nyaraka za fedha.

“ Kwa kweli mimi nahisi hawataki niingie katika uchaguzi huo kamati imenitaka nikabidhi nyaraka hizo Jumatano wakati leo (jana) ni Jumamosi hakuna kazi, kesho (leo) Jumapili, Jumatatu hadi Jumanne ni sikukuu na Jumatano nikabidhi kwa ajili ya kuhojiwa tena Alhamisi na kama nikipita nitapata wapi muda wa kujiandaa na nikishindwa nitapata wapi muda wa kukata rufaa…’’ alisema Wambura.

Alihoji kwa nini kamati imeamua kupeleka mbele suala lake kiasi hicho nia ni kumuharibia ili asiweze kujiandaa katika uchaguzi huo au kutoingia kabisa katika uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment