
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametunukiwa Shahada ya Uzamivu (PHD) ya Heshima na Chuo Kikuu cha Kenyatta cha Kenya kwenye mahafali ya 25 ya chuo hicho yaliyofanyika kwenye chuo hicho nje kidogo ya Jiji la Nairobi.
Dk Kikwete alikuwa miongoni mwa watu watatu mashuhuri ambao wametunukiwa shahada hiyo ya uzamivu ya heshima kwenye mahafali hayo yaliyohudhuriwa na mamia ya wasomi, wahitimu wa shahada, stashahada na vyeti pamoja na wazazi wao na jamaa zao. Jumla ya wahitimu 3, 417 wametunukiwa shahada, stashahada na vyeti wakiwamo 23 ambao wametunukiwa shahada za uzamivu katika masomo mbali mbali na 312 ambao wametunukiwa shahada ya uzamili.
Wengine ambao wametunukiwa shahada hiyo ni Makamu wa Rais wa Kenya, Stephen Kalonzo Musyoka, na msomi na mdau mkubwa wa elimu katika Kenya, Dk. Eddah Wacheke Gachukia.
Rais Kikwete na Makamu wa Rais Musyoka wametunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Doctor of Humane Letters wakati Dk. Gachukia ametunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Doctor of Education, Dk Kikwete ametunukiwa shahada hiyo ya uzamivu kwa sababu tatu.
Sababu ya kwanza ni uongozi uliotukuka kuanzia alipokuwa kiongozi wa wanafunzi kwenye Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam katika miaka ya 1970 hadi alipofanikiwa kuwa Mtanzania wa kwanza kushika wadhifa wa uwaziri wa fedha katika umri mdogo zaidi kuliko Mtanzania mwingine katika historia ya Tanzania huru.
Kwenye nafasi hiyo, Dk Kikwete alifanya mageuzi makubwa katika muda mfupi aliokaa katika wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuleta nidhamu na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma. Alikuwa ni yeye aliyeanzisha utaratibu wa Serikali kutumia kile ilichokikusanya (cash budget), na pia kuanzisha maandalizi ya uundwaji wa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA).
Miongoni mwa mafanikio yake makubwa ya uongozi ni mchango wake mkubwa katika kufufuliwa kwa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC). Akiwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuia ya Afrika Mashariki, aliongoza mchakato wa kuundwa kwa Umoja wa Forodha wa EAC miongoni mwa nchi tatu wanachama wa awali wa Jumuia hiyo- Tanzania, Kenya na Uganda.
Katika maelezo yake kuelezea kwa nini alistahili kupewa shahada hiyo, uongozi wa chuo hicho ulisisitiza kuwa hata katika nafasi yake ya sasa ya Uenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) anaendelea kuonyesha mifano ya kuigwa ya uongozi. Dk Kikwete pia ametunikiwa shahada hiyo kutokana na mchango wake mkubwa katika kutafuta amani hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, Rais Kikwete alitoa mchango mkubwa kutafuta amani katika Eneo la Maziwa Makuu, na hasa katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Katika Kenya yenyewe, Rais Kikwete aliongoza jitihada za AU katika kurudisha amani na maelewano katika nchi hiyo kufuatia mauaji na machafuko makubwa yaliyoikumba nchi hiyo Januari, mwaka huu, kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini humo Desemba mwaka jana, 2007.
Sababu ya tatu kwa nini Chuo Kikuu cha Kenyatta kimemtunukiwa shahada hiyo Dk Kikwete ni kutokana na mchango wake mkubwa katika kuinua na kupanua kiwango cha elimu katika Tanzania kwa namna ambayo ilikuwa haijapata kutokea katika historia ya Tanzania katika kipindi kifupi. Katika miaka mitatu ya uongozi wake, Rais Kikwete amefanikiwa kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Kitanzania aliyeshinda mtihani wa darasa la saba anaingia sekondari.
Matokeo yake ni kwamba idadi ya wanafunzi wa sekondari imeongezeka kutoka wanafunzi nusu milioni hadi kufikia milioni 1.2 katika miaka mitatu iliyopita na pia kuongeza idadi ya sekondari mara tatu kutoka shule 1, 202 mwaka 2005 hadi kufikia 3, 039 mwaka huu, kutokana na sera ya ujenzi wa angalau shule moja ya sekondari kila kata ya Tanzania.
Baraza la Chuo Kikuu na Baraza la Seneti la Chuo Kikuu cha Kenyetta pia vimesema kuwa vimefikia uamuzi wa kutoa shahada hiyo kwa Rais Kikwete kwa sababu ya mchango wake katika kupanua kwa kiwango kikubwa elimu ya juu katika Tanzania, hasa uamuzi wake kujenga chuo kikuu kipya cha Dodoma.
Chuo Kikuu cha Dodoma kitakuwa chuo kikubwa zaidi nchini Tanzania kikiwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 40,000 kwa wakati mmoja na kilianza kwa uamuzi binafsi wa Rais Kikwete mara tu baada ya kuwa ameingia madarakani mwaka 2005.
Chuo Kikuu cha Kenyatta pia kimemwagia sifa nyingi Rais Kikwete kwa juhudi zake za kupambana na rushwa katika Afrika, na hasa katika Tanzania. Hii ni shahada ya pili ya uzamivu kutunukiwa Rais Kikwete.
Mwaka 2006, Rais alitunikiwa shahada ya uzamivu na Chuo Kikuu cha St. Thomas cha Jimbo la Minesotta katika Marekani. Rais Kikwete aliwasili mjini Nairobi, Kenya jana, Alhamisi, Desemba 18, 2008 Ends
No comments:
Post a Comment