![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhakHWxlVC-lNmFVllxCd3c886Jv5zK0Da6oqStePxEHrf26Wce_6NXyoSBtO7h9B4af3idfkBh5lC_h7KtbCgG_8pR-K6pelUGf3gXWToX83_kI9ZPjcxqOcrHua0HXvrSBedEJ1vY6To/s320/_matakaa.jpg)
HIRIKA la Ndege (ATCL) limekiri kuwa licha ya kukaguliwa na kitengo cha ukaguzi cha Chama cha Kimataifa cha Usafiri wa Anga (IOSA) tangu Desemba mwaka jana, lilishindwa kukidhi utashi wa viwango vipya vya usafiri huo na kusababisha linyang'anywe cheti cha kuendesha shughuli zake na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).
Kutokana na kunyang'anywa cheti hicho kinachoitwa AOC (Air Operations Certificate), shirika hilo limesema litakuwa likikosa karibu Sh300 milioni kwa wiki katika kipindi ambacho litakuwa halifanyi safari za anga kusubiri TCAA kufanyia kazi nyaraka zilizowasilishwa na ATCL juzi.
ATCL imezuiwa kufanya safari za anga baada ya TCAA kuinyang'anya cheti cha usafiri huo tangu Desemba 8 baada ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) kukagua shughuli za TCAA Novemba mwaka huu na kubaini nyaraka za ATCL zilizokuwa kwenye mamlaka hiyo ya Tanzania hazikuwa zikiendana hata na sheria za TCAA za mwaka 2006 na hivyo kushauri linyanyang'anywe cheti hicho kwa muda usiojulikana.
Ukaguzi huo wa ICAO umekuja baada ya IOSA kufanya ukaguzi mwingine Desemba mwaka 2007 na kubaini jumla ya dosari 482 ambazo hazikufanyiwa kazi na ATCL hadi ukaguzi mwingine ulipofanyika mwezi uliopita.
"Novemba mwaka 2008, ICAO ilikuja nchini kukagua jinsi TCAA inavyofanya shughuli zilizo chini yake za kuangalia mashirika ya ndege yanayofanya kazi nchini," alisema mkurugenzi mkuu wa ATCL, David Mattaka katika mkutano wake na waandishi wa habari jana.
"Katika kufanya hivyo, (ICAO) walibaini kuwa zile nyaraka za kiutaratibu ambazo zilikuwa TCAA, hazikulingana na sheria za TCAA za mwaka 2006. Nyaraka hizo ndio zile ambazo zilikuwa zikiandikwa upya ili ziendane na sheria mpya," aliongeza Mattaka.
"Kwa maana hiyo, walibaini kuwa cheti cha AOC kilichokabidhiwa kwa ATCL na ambacho muda wake ulitakiwa kuisha Desemba 15, 2008, hakikutolewa kwa kufuata utaratibu. Kwa hiyo, TCAA iliamua kunyang'anya AOC hadi hapo ATCL itakapokamilisha nyaraka na kukidhi utashi wa TCAA."
Akijibu swali juu ya sababu zilizoifanya ATCL ishindwe kukamilisha utashi wa viwango vya usafiri wa anga tangu Desemba mwaka 2007 wakati IOSA ilipobaini mapungufu hayo 482, Mattaka alisema hiyo ilitokana na kampuni walizoziteua kuwashauri kiufundi kutoka nje ya kushindwa kukamilisha kazi yao hadi siku ya mwisho ya muda ambao TCAA iliwapa ATC ambayo ilikuwa juzi.
Hata hivyo, Mattaka alisema tayari shirika lake limeshakamilisha nyaraka hizo na kuziwasilisha TCAA, ambayo imeahidi kwa maneno kuwa inahitaji siku kumi za kazi ili iweze kuzishughulikia na kuirudishia ATCL cheti hicho cha usafiri wa anga.
Shirika hilo limekuwa taaban tangu ndoa yake na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) ivunjike, likiwa linashindwa kusafirisha wateja wake mara kwa mara, kukataliwa kujaza mafuta wakati ikiwa nje kutokana na kudaiwa na kampuni ya mafuta ya BP na kupungukiwa na ndege kutoka tano hadi mbili baada ya tatu kuharibika.
Akifafanua matatizo hayo, Mattaka alisema katika dosari 482 ambazo IOSA ilibaini, 39 zilikuwa katika muundo na menejimenti, dosari 206 zikiwa katika safari, huku dosari 55 zikiwa katika huduma ya mizigo.
Alitaja dosari nyingine kuwa katika maeneo ya matengenezo (45), wahudumu (7), huduma baada ya kutua (50), utumaji mizogo (44), na usalama wa uendeshaji ambao ulikutwa na dosari 36.
Mattaka alisema kutokana na matakwa ya TCAA tayari ATCL imeshafanyia kazi nyaraka hizo na kuziwasilisha TCAA tangu juzi na inasubiri ahadi ya mamlaka hiyo kuzishughulikia katika muda wa siku kumi za kazi.
"Tungependa kusisitiza kuwa matatizo katika nyaraka hayahusiani na usalama wa safari za ndege na wasafiri hawajawahi kuwa hatarini kutokana na matatizo (hayo ya nyaraka)," alisema Mattaka, ambaye alikuwa mkurugenzi mkuu wa Mfuko wa Pensheni ya Mashirika ya Umma (PPF).
Kuhusu ahadi ya kuisaidia ATCL iondokane na mzigo wa matatizo hayo, Mattaka alisema serikali ina nia ya kulisaidia shirika hilo kwa dhati, lakini ili kuisaidia ni lazima itumie kodi za wananchi au kutafuta mwekezaji.
Alisema kuna kampuni ya Kichina ambayo inataka kulichukua shirika hilo na mazungumzo na serikali yanaendelea.
Mattaka alisema gharama za uendeshaji mashirika ya ndege ziko juu sana, akitoa mfano wa uendeshaji wa ndege aina ya Airbus kutoka Dar kwenda Mwanza na kurudi inagharimu kiasi cha Sh9 milioni wakati kurusha ndege aina ya Boieng hugharimu Sh10 milioni.
'Tunashukuru bei ya mafuta imepungua na gharama pia zimepungua," alisema Mattaka.
Wakati shirika hilo likiingia katika hasara hiyo, wateja wake ambao walikuwa wamekata tiketi kwa ajili ya safari kuelekea maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi kabla ya ATCL kusimamishwa watarudishiwa fedha zao ili waweze kutafuta usafiri mwingine.
Naye Waziri wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa alisema ATCL ilistahili adhabu hiyo ya kunyang'anywa cheti cha usafiri wa anga kutokana na kukiuka baadhi ya vipengele vya sheria.
Alisema kwa kawaida masuala yote ya anga yanasimamiwa na Chama cha Kimataifa cha Usafiri wa Anga (IATA) na kwamba baada ya chombo hicho kufanya ukaguzi, kilibaini makosa ya kiufundi yanaweza kusababisha athari, lakini wao ATCL hawayashughulikia.
Lakini alisema serikali imeshaingilia kati suala hilo na kwamba kuna baadhi ya marekebisho yanafanywa ili kulinusuru liweze kurudi katika hali yake ya kawaida.
Alisema pamoja na marekebisho hayo pia serikali ipo kwenye mchakato wa maongezi na muwekezaji mpya ambaye ameonyesha nia ya kuwekeza katika shirika hilo.
No comments:
Post a Comment