KARIBU SANA

Wednesday, December 3, 2008

Mtuhumiwa wa EPA aliyebaki apata dhamana

Mtuhumiwa wa pekee wa kesi ya wizi wa fedha za kaunti ya madeni ya Nje (EPA) aliyekuwa amebaki rumande hatimaye apata dhamana

HATIMAYE mtuhumiwa wa ufisadi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Imani Mwakyosa ambayeb alikuwa amebaki jana alipata dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa na mahakama.

Mtuhumiwa huyo ambaye ni mmoja wa wakuu wa Idara ya Madeni ya Biashara BOT alipandishwa kizimbani Novemva 7 mwaka huu akiwa na wenzake lakini alijikuta kwa zaidi ya wiki tatu akishindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Mwakyosa na wenzake wanadaiwa kuwa wazembe wakiwa kazini na kulisababishia taifa hasara ya Sh 207 milioni.

Hakimu Mkazi Hezron Mwankenja anayesikiliza kesi hiyo aliweka masharti ya dhamana kwa mshitakiwa huyo ambapo alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, kuwasilisha mahakamani hati yake ya kusafiria na kutoa pesa taslimu Sh 26 milioni.

Mshitakiwa huyo alishindwa kutimiza sharti la kutoa pesa taslimu Sh 26 milioni na kukata rufaa Mahakama Kuu akiomba kulegezwa kwa sharti hilo ili aweze kutoa hati ya mali yenye thamani ya pesa hizo.

Mahakama kuu ilikubali kulegeza masharti ya dhamana kwa mshitakiwa huyo na kuelekeza atoe pesa taslimu ama hati ya mali yenye thamani sawa na kiasi hicho cha fedha.

Mshitakiwa huyo jana alitimiza masharti hayo ambapo alitoa hati ya mali yenye thamani ya Sh 106 milioni na kuachiwa huru. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 20 mwakani.

Wakati huo huo, upande wa mashitaka katika kesi ya ufisadi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) inayomkabili Japhet Lema umedai kuwa una mpango wa kuongeza mshitakiwa mwingine.

Wakili wa serikali Thadeo Mwenempasi alidai mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Euphamia Mingi kuwa uchunguzi bado unaendelea na kuomba kesi hiyo iahirishwe hadi Januari 30 mwakani.

Lema alipandishwa kizimbani kwa tuhuma za kujipatia zaidi ya Sh 2 bilioni kutoka katika kampuni ya Njaki na Itoh ya nchini Japan baada ya kuwasilisha hati ya uongo.

No comments:

Post a Comment